Home > Featured_Slider > Mwenyekiti Wa Bodi Ya Parole Mrema Ataja Mambo Manne Kumaliza Mauaji Rufiji Na Kibiti

Mwenyekiti Wa Bodi Ya Parole Mrema Ataja Mambo Manne Kumaliza Mauaji Rufiji Na Kibiti

Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Augustino Mrema amependekeza kufanyika kwa mambo manne haraka iwezekanavyo ili kumaliza matukio ya mauaji yanayoendelea Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.
Mrema ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani miaka ya 1990, aliitaka Serikali isiogope gharama ili kudhibiti tatizo hilo lisienee maeneo mengine.

 
Mrema ambaye wakati wa utawala wake aliwahi kuamuru majambazi wasalimishe silaha kwa hiyari yao na wakasalimisha, alisema polisi kwenda na silaha nzito inaweza isisaidie kuwapata wahusika.
Ushauri huo wa Mrema, umekuja wakati kukiwa na mfululizo wa mauaji katika maeneo hayo na tukio jipya likiwa la mauaji ya askari wawili wa kikosi cha usalama barabarani yaliyotokea juzi Bungu, Kibiti.
Kuuawa kwa polisi hao kulikoambatana na gari lao kuchomwa moto, kunafanya idadi ya askari waliouawa kwa risasi mkoani Pwani kufikia kumi na moja kati ya Januari 2015 na Juni 21 mwaka huu.

 
Tukio la kwanza lilitokea Januari, 2015 katika kituo cha Polisi cha Ikwiriri ambako majambazi waliovamia kituo hicho waliwaua polisi watatu na kupora bunduki za kivita ndani ya kituo hicho.
Februari mwaka huu, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya aliuawa pamoja na watu wengine wawili na Aprili 9 wakauawa polisi watatu waliokuwa katika kizuizi.

 
Lakini tukio baya zaidi likatokea Aprili 13, baada ya polisi wanane kuuawa kwa mpigo baada ya kushambuliwa kwa risasi walipokuwa wanarejea kambini na bunduki saba kuibwa.
Wauaji hao hawakuwalenga tu polisi, kwani katika mfululizo wa matukio ya mauaji, wapo viongozi wa vijiji, wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na raia wa kawaida waliouwa mkoani Pwani.

 
Ushauri wa Mrema
Mrema alisema Serikali inapaswa kuwekeza katika intelijensia zaidi kwa kupandikiza watu katika maeneo hayo ili kukusanya taarifa zitakazolisaidia Jeshi la Polisi.
“Namna ya kuwajua hao watu ni kupandikiza watu, ukienda na magwaride na mabunduki hadharani pengine ni suluhisho la muda mfupi tu. Suluhisho ni kupandikiza watu kwa siri,” alisema Mrema.

 
Mrema aliitaka Serikali kutoogopa gharama katika jambo hilo na ipandikize watu ambao itawachuja kwa umakini mkubwa, kwani kwa jinsi inavyolishughulikia, inaweza isizae matokeo kwa haraka.
Mbali na ushauri huo, lakini Mrema aliitaka Serikali kuchunguza historia ya maeneo hayo, ili kubaini kama kuna vijana waliosafirishwa kwenda nje kupata mafunzo mabaya na ya matumizi ya silaha.
Mrema alisema kwa maoni yake, wanaofanya mauaji hayo si wahalifu wa kawaida kutokana na ujasiri wa kuwakabili polisi walionao na pia namna wanavyolenga shabaha na walivyo na utaalamu wa silaha.

 
Alishauri washukiwa wote walioko mikononi mwa polisi, watumike kama chanzo cha kupata habari ya nini kinachoendelea katika maeneo hayo, kwa sababu gani na nani wanayafanya.
“Tutumie gharama kwa sababu jambo hili litaenea na litatugharimu. Hao ambao tumeshawakamata tukae nao wawe ni chanzo cha taarifa muhimu. Tukiliachia hilo jambo linavyoenda ni hatari,” alisema.
“Mkuu wa polisi aliyekuwapo (Ernest Mangu) amepiga kelele mpaka ameondolewa. Amekuja huyu mpya (Simon Sirro) amepiga kelele. Rais (John Magufuli) amesema jana (juzi) tu na wameua tena.
“Pale kuna mchezo unachezewa nchi hii na unaanzia Kibiti na Rufiji. Vyombo vyetu vifungue macho. Kuna kundi linataka ku destabilize (kuvuruga) usalama wa nchi ili wafanye yao. Tusikubali.
“Mimi nina wasiwasi hao wanaoua watu sio wahalifu wa kawaida. Nina wasiwasi kuna vijana wamepelekwa … na … kwa miaka iliyopita wakapata mafunzo mabaya,” alisema Mrema.

Jambo jingine ambalo Mrema alishauri, ni kwa Polisi kuwatumia viongozi wa kidini na kisiasa kujaribu kurudisha uhusiano kati ya raia na polisi ili waweze kushirikiana nalo katika vita hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *