Home > Featured_Slider > Dkt. Shein: Bei Ya Karafuu Kutoshuka 

Dkt. Shein: Bei Ya Karafuu Kutoshuka 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesema Serikali haijaona sababu ya kushusha bei ya ununuzi wa karafuu kutokana na wakulima kuimarisha kilimo cha zao hilo.

Dkt Shein amesema hayo akizungumza na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) na watendaji wa ofisi hizo Ikulu mjini Zanzibar.

Amesema jitihada za wakulima zinatokana na mageuzi yaliyofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka sita iliyopita kuanzia 2011, kwa kupandishwa bei ya karafuu kwa wakulima kutoka Sh5,000 hadi Sh14,000 kwa kilo moja.

Ameahidi Serikali itazidi kuunga mkono jitihada za wakulima kwa kadri hali itakavyoruhusu.
“Ni wazi kuwa sheria mpya ya ZSTC ya mwaka 2011, Sheria ya Maendeleo ya Karafuu ya mwaka 2014 na Mageuzi ya miaka 10 (2011-2021) ya Shirika la ZSTC yametimiza lengo la Serikali la kuliimarisha zao la karafuu na matunda yake yameanza kuonekana,” amesema.

Dkt. Shein amesema Serikali kupitia ZSTC imeimarisha zaidi huduma kwa wakulima ikiwemo ujenzi wa vituo vya ununuzi ambavyo vipo 32 Unguja na Pemba.

Amesema mikopo inayotolewa bila ya riba kwa wakulima, miche ya mikarafuu na elimu juu ya uimarishaji wa zao hilo ni juhudi zinazofanyika za kuendeleza kilimo cha karafuu.

Dkt. Shein amesema ili kuendelea kuwaenzi wakulima na kuhakikisha wanauza karafuu serikalini bila ya shida, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo yenye karafuu nyingi .

Ameitaka Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa ZSTC kuzisoma na kuzifahamu vyema sheria zinazoongoza sekta ya karafuu ili kutekeleza vyema majukumu ya uendelezaji wa zao hilo.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC, Dk Said Seif Mzee amesema katika utekelezaji wa mageuzi, shirika limejizatiti katika uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na la nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *