Home > Featured_Slider > Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Atembelea Mtambo Wa Kusafisha Dhahabu Mkoani Mbeya.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Atembelea Mtambo Wa Kusafisha Dhahabu Mkoani Mbeya.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametembelea na kujionea mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu kwa asilimia 99 unaomilikiwa na kampuni ya Sunshine Group uliopo katika kata ya Matundasi wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Ametembelea mtambo huo leo Jumanne, Agosti 1, 2017 wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya na kusema kuwa mtambo huo ni wa kwanza kuweza kusafisha dhahabu kwa kiwango hicho hapa nchini.

Amesema kwa Tanzania kampuni ya Sunshine Group ndiyo yenye mtambo wa kuweza kusafisha dhahabu na kufikia asilimia 99 ukilinganisha na makampuni mengine yanayomiliki migodi.

Pia Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza katika mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchenjulia makinikia ili kuweza kusafirisha dhahabu halisi.

Naye Ofisa Madini Mkoa wa Mbeya, Mhadisi Said Makwama, amesema dhahabu inayosafishwa katika mtambo huo ikipelekwa nje ya nchi inaingizwa sokoni moja kwa moja tofauti na ile inayotoka katika migodi mingine.

Mhandisi huyo amesema sheria mpya ya madini imesaidia Serikali kupata kodi ya juu itokanayo na mrabaha wa asilimia 6 na kodi ya ukaguzi ya asilimia moja ya thamani ya madini yanayosafirishwa ukilinganisha na mrabaha wa awali wa asilimia nne.
“Kwa uzalishaji uliofanyika kwa mwezi Julai tu Serikali imepata mrabaha wa Sh333 milioni ukilinganisha na sheria ya zamani Serikali ingepata Sh191 milioni.

Kwa upande wake mbunge wa Chunya, Victor Mwambalaswa, ameiomba Serikali kukubali maombi ya Kampuni ya Sunshine ya kujenga mtambo wa kuchenjulia mabaki ya mchanga wa dhahabu wilayani Chunya ili kuweza kuongeza fursa za ajira, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *