Home > Bunge > KAULI YA SERIKALI KUHUSU WAPANGAJI WANAOLIPA KODI ZA NYUMBA KWA MIEZI 6 AU MWAKA

KAULI YA SERIKALI KUHUSU WAPANGAJI WANAOLIPA KODI ZA NYUMBA KWA MIEZI 6 AU MWAKA

Baada ya wananchi kulalamika kwa muda mrefu, serikali imesikia kilio chao na kusema kuwa ipo katika mchakato wa kuandaa sheria ambayo itaondoa utaratibu wa kulipa kodi ya pango kwa miezi sita au mwaka katika nyumba za makazi.

Hayo yalisema jana Novemba 17 bunge na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum CCM, Halima Bulembo aliyetaka kujua ni lini serikali itatunga sheria itakayompa nafasi mpangaji kulipa kodi ya mwezi mmoja badala ya utaratibu wa sasa wa miezi sita au mwaka.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri alonukuliwa akisema, “Wizara tayari imeshaliona hilo na tupo kwenye mchakato wa kuanzisha mamlaka itakayosimamia masuala yote ya nyumba, katika sheria inayoandaliwa kwaajili ya kuletwa bungeni imeangalia ukomo wa kutoa kodi hivyo hiyo ya miezi sita haitakuwepo.”

Naibu Waziri Mabula aliongeza kuwa, baada ya sheria hiyo kupitishwa kodi itakuwa inatolewa kwa mwezi mmoja mmoja badala ya utaratibu wa sasa unaoumiza wananchi wa kodi kulipwa kwa mwaka au nusu mwaka.
“Kodi itakuwa inatolewa kwa mwezi mmoja wakati huo mpangaji atalazimika kutoa amana ya miezi mitatu kwaajili ya mambo mengine yanayoweza kujitokeza.”

Kwa miaka mingi wananchi mbalimbali wamekuwa wakilalamikia utaratibu uliowekwa na wamiliki wa nyumba za makazi wa kuwataka kulipa kodi ya miezi 6 au mwaka kutokana na hali zao za kipato kuwa duni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *