Home > Featured_Slider > HOSPITALI YA MLOGANZILA KUPUNGUZA RUFAA TIBA NJE

HOSPITALI YA MLOGANZILA KUPUNGUZA RUFAA TIBA NJE

Kukamilika kwa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili(MUHAS) iliyojengwa  katika eneo la Mloganzila pembezoni mwa jiji la Dar es salaam na mkoa wa pwani ni matokeo chanya ya juhudi za Serikali za Tanzania ikiwemo ya Awamu ya Tano.

Hospitali hii imepewa hadhi ya Rufaa ya Taifa (National Super Specialized Hospital) ina uwezo wa kutoa huduma za matibabu za kibingwa, kufundisha wataalam wa huduma za afya. Hospitali ina vifaa vya kisasa vya kuchunguza magonjwa ya aina mbali mbali na kutoa matibabu ya hali ya juu.

Ujenzi wa MAMC pamoja na Kampasi ya Mloganzila ulipewa kipaumbele cha juu na serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa eneo hili na kutenga fedha za malipo ya fidia ya mali(TZS 10,741,692,489.63) kwa wakazi 2,665 wa maeneo ya Mloganzila ,Kwembe, Kisopwa na King’azi ili kupisha ujenzi.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila ilianza kwa ujenzi wa hositali ya kisasa kabisa ya Taaluma na Tiba, ambapo ujenzi ulizingatia jukumu la mafunzo wakati ikitoa Tiba zenye kiwango cha kimataifa.

Gharama ya ujenzi wa hospitali hii pamoja na kuiwekea vifaa na mfumo wa TEHAMA ni Dola za Kimarekani 94,540,000 ambapo Dola za Kimarekani 76,500,000 ni mkopo kwa Serikali wa masharti nafuu kutoka kwa Serikali ya Korea kusini na Dola za Kimarekani 18,040,000 zimetolewa na Serikali ili kukamilisha ujenzi huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mradi huu unafanikiwa na kukamilika.Juhudi zake zimedhihirika toka kipindi alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kufanya juhudi kuwezesha upatikanaji wa eneo la Mloganzila.

Aidha, alipoingia tu Ikulu mwaka 2015, alihakikisha kuwa kiasi cha fedha takribani bilioni 23 zilizokuwa zimebaki katika ahadi ya Serikali kwa ujenzi wa Hospitali hii zinapatikana na kumlipa mkandarasi kwa wakati.Hii iliwezesha mkandarasi kukamilisha ujenzi wa hospitali kwa wakati bila kusimamisha kazi.

Hospital hii ina ghorofa tisa zenye uwezo wa vitanda 571, vyumba vya upasuaji 13, viwili(2) kati ya hivi vikiwa kwa ajili ya upasuaji wakati wa uzazi, na kimoja kikiwa kwa ajili ya upasuaji wa dharura na majeruhi. Ujenzi wake ulizinduliwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne Mhe Dkt Jakaya Mrisho Kikwete Aprili 24,2014 na Rais Dkt Magufuli alitarajiwa kuzindua rasmi utendaji kazi wa Hospitali kufikia Novemba, 2017. Ujenzi ulikamilika tarehe 13 Agosti mwaka 2016 kama ilivyokuwa imepangwa na vifaa tiba vilianza kuwekwa sehemu zote husika. Vifaa Tiba vilivyopo ni pamoja na mashine za CT scan, MRI, vifaa vya kusafisha damu kwa wagonjwa wenye magonjwa ya figo na mitambo ya kusafirishaji sampuli za uchunguzi. dawa na  majibu ya vipimo vya magonjwa kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kutumia msukumo wa hewa.

Vifaa pamoja na miundombinu iliyopo katika hosipitali ya MAMC vitawezesha utoaji wa mafunzo yenye ubora, utoaji wa huduma za matibabu yaliyo bora, uchunguzi wa magonjwa na kufanya tafiti za fani za afya zilizo bora hapa nchini. Hospitali itatoa huduma nyeti na adimu katika ukanda huu wa Afrika kutokana na uwezo wa wataalamu wake na italiepusha Taifa na rufaa nyingi za nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *