Home > Featured_Slider > SALAAM ZA NDG. SHAKA HAMDU SHAKA (MNEC) 2018

SALAAM ZA NDG. SHAKA HAMDU SHAKA (MNEC) 2018

*********************************

TANZANIA INAHESHIMU UHURU, KATIBA NA SHERIA!

Siku zote uongozi usioheshimu sheria na Katiba ya nchi huwa ni uongozi wa kidikteta. Tanzania haijawahi kuwaza, kufikiria wala kujaribu kutenda au kufanya mambo ya kidikteta.

Serikali zetu zote kwa SMZ na JMT zimeheshimu na kufuata misingi ya utawala wa sheria bila kuvunja  aidha Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1984 na ile ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania ya mwaka 1977. Serikali zetu hazijawahi kuonyesha dalili za uimla .

Ndio maana hata baadhi ya mawazo ya wakosoaji, hutoa mawazo huku wakibaki huru kwa kuamini nchi yetu inaheshimu sheria na kuenzi haki za binadamu. Aidha katika suala la uhuru wa kuabudu nalo  liko wazi kwani Serikali zetu zingekuwa haziheshimu sheria au kutofuata matakwa ya Katiba ya nchi, ingeamua watu wote wawe waumini wa dini na dhehebu moja na suala la kuabudu lifutwe jambo ambalo si sahihi. Licha ya baadhi ya viongozi wa dini wakati mwingine kuutumia uhuru huo wa kuabudu kwa kujihusisha na siasa huku wakiishambulia Serikali kwa hoja dhaifu bado Serikali imekuwa na uvumilivu mkubwa wa kuheshimu maoni yao.

Ikiwa Viongozi wa dini wataendelea kutimiza wajibu wao wa kuhubiri maneno ya Mwenyezi Mungu na kueneza maandiko matakatifu ya kiroho kwa jamii, tutajenga  taifa la wananchi wenye upendo, umoja, mshikamano, maadili na wenye  hofu kwa Mungu. Hivyo basi vitendo viovu kama matumizi ya dawa za kulevya, ujangili, rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma vitapungua na amani yetu itadumu milele.

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tunawatakia heri ya mwaka mpya 2018 na kuwaomba watanzania wenzetu ambao ni watumishi wa umma, wanasiasa, watendaji wenye dhamana serikalini, mashirika ya hiari ya kijamii na yasiokuwa ya kiserikali, waendelee kutimiza wajibu huo kwa ufanisi, weledi na umakini huku tukiwahimiza viongozi wetu wa dini wabaki kuwa walezi wa mioyo ya imani, kuhubiri upendo na uzalendo kwa Taifa letu si vinginevyo.

UVCCM tunaamni Serikali zetu zote mbili zimekuwa zikiheshimu dhana ya kukubali kukosolewa, kujikosoa na kujisahihisha. Masuala yote ya msingi yatasikilizwa, yatachukuliwa kwa umuhimu wa kipekee ili kufanyiwa kazi ipasavyo tena kwa mwendo wa haraka. Tukiamua kuweka kando tabia ya ushabiki, ubishi, ukaidi na unazi, tutalijenga Taifa letu sisi wenyewe na kujiletea maendeleo ya kujivunia.

Mwisho, Tanzania ni nchi yetu sote tuna haki na wajibu wa kuipenda , kuitetea, kuipigania kisiasa , kiuchumi na kijamii kwa kutumia nguvu, akili, maarifa na kuonyesha bidii, juhudi na uthubutu. Tuipende, tuilinde, tuitetee na kuijenga kwa nguvu zetu zote.

*Mungu Ibariki Tanzania.

*Mungu Ibariki Afrika na watu wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *